A song made by Sir Nixy
A song made by Sir Nixy
Intro
Sir Nixy
Yeah...Uhm
Hii ni sauti ya baba yenu iliyochoka,yenye mtetemeko wa unyonge na maumivu!
Naanza kwa kusungumza maneno haya kwa Sauti ya Usemi!
"Greda likimaliza kazi ya kupasua miamba mlimani....
Njia ikishanyooka na kua lami safi...
Huwa hawairuhusu kupita juu yake tena.
Wanasema chuma chake kitaharibu uzuri wa barabara hiyo...
Wanalipakiza kwenye tela lingine katili,wanalitupa kwenye yadi likaliwe na kutu...
Uhm.....hehe! Sikitiko...
Hivi ndivyo ilivyo sacrifice ya baba...
Nilikata miiba mkanikanyaga mgongoni mkavuka.
Leo nimebaki gofu...barabara mnafurahia town,baba yenu mmenitupa kwenye banda la mbuzi...
Ee mola wangu...sikia kilio hiki"
Verse 1
Nilikodisha mabega yangu kuwa rula ya nyika
Nikalima miiba kwa kucha,mapori yakanyooka.
Nikalala uchi ili mawingu yawavishe magwanda ya hariri,
Nikameza shubiri ya njaa,ili vinywa vyenu vionje asali ya elimu.
Nilikua mzizi uliosimama gizani chini ya ardhi,
Ili matawi yenu yachanue maua na kuitwa matunda mlimani.
Verse 2
Kisima nilichochimba kwa mifupa na mikopo ya damu,
Leo kimejaa maji,lakini nanyimwa hata tone la koo.
Nilikata mianzi nikajenga ghala za kifahari town,
Mke niliyempa funguo,akabadili kufuli ghafla.
Nikadhani nimepanda mbegu ya mkaratusi initunze uzeeni,
Kumbe nilipalilia mti wa miiba,utakaonichoma macho nikiwa kipofu.
Chorus
Mbona sacrifice ya baba ni mfano wa fumbo la Greda?
Huvunja miamba na vilima,ikatandaza barabara safi ya lami,
Lakini lami ikishang'aa,mashine hiyo ikikanyaga tu inaitwa haramu,
Wanasema itaharibu njia,wanaipakiza juu ya tela lingine katili!
Niligeuza mgongo wangu barabara,leo miguu yangu haina haki ya kupita.
Verse 3
Yule nzi niliyemkingia dhoruba asizame kwenye maziwa
Leo amekua nyuki,anawadunga wanangu sumu ya kunichukia.
Amewafundisha kusahau alama za viganja vyangu vilivyokakamaa,
Anawaambia mti uliowazaa haukuwahi kua na kivuli.
Mwanangu niliyemshika mkono akajua herufi za kwanza,
Leo anasoma barua yangu ya kilio kama karatasi la takataka.
Verse 4
Nguvu zangu zimefifia,jua la jioni limefika limebeba maradhi,
Mwili unatafunwa na moto wa ndani,presha na sukari vimekua dhoruba.
Wale niliowajengea majumba ya ghorofa na vioo vya mamlaka,
Wamenitupa pembeni,kwenye kibanda cha mbuzi kisicho na mlango.
Baridi ya usiku inanichambua kama pamba,huku nikitetemeka,
Wakati nyumba zangu nilizojenga kwa mkopo zikiliwa na wageni mjini.
Chorus
Mbona sacrifice ya baba ni mfano wa fumbo la Greda?
Huvunja miamba na vilima,ikatandaza barabara safi ya lami,
Lakini lami ikishang'aa,mashine hiyo ikikanyaga tu inaitwa haramu,
Wanasema itaharibu njia,wanaipakiza juu ya tela lingine katili!
Niligeuza mgongo wangu barabara,leo miguu yangu haina haki ya kupita.
Outro
Nilisafisha nyika...mkapata njia ya kwenda mjini.
Mkajenga minara...mkasahau udongo ulioshikilia misingi yenu.
Mimi ndio Greda lenu...lililotupwa mbali baada ya kazi kukamilika.
Mungu asikie kilio cha huku banda la mbuzi...
Woooi!...woooi!
Umh.....!